NJAA YA WAKUMBA WAATHIRIKA WA BOMOABOMOA









Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na
Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba,  akizungumza na mmoja wa waathika wa nyumba zilizobomolewa katika Bonde la Mkwajuni, Dar es Salaam alipotembelea eneo hilo jana. Picha na  Mpigapicha Wetu 
By Jackline Masinde, Mwananchi
Dar es Salaam. Wakazi wa bonde la Mkwajuni Manispaa ya Kinondoni jijini hapa, waliobomolewa nyumba zao wanaomba msaada wa chakula kutoka kwa wasamaria wema.
Wakiwa katika vifusi vilivyotokana na nyumba zao kuvunjwa, waathirika hao walisema wanashindia maji na uji huku wengine wakilala na njaa kutokana na kukosa fedha za kununulia chakula.
Walisema wengine wamegeuka ombaomba kwa ndugu na jamaa zao wa karibu baada ya kukosa fedha, vyakula na mahali pa kuishi tangu walipovunjiwa nyumba zao.
Wakizugumza na mwandishi wa gazeti hii alipotembelea eneo hilo mwishoni mwa wiki, walisema hali ya maisha kwa upande wao ni ngumu kwa kuishiwa fedha na kukosa uwezo wa kununua chakula, hivyo kuwa hatarini kufa kwa njaa.
“Dada tunakufa na njaa...tumesuswa, tunaishi maisha ya kubahatisha leo ukipata unakula, kesho ukikosa unalala, tumegeuka ombaomba mpaka ndugu wengine wanatuchoka,” alisema Erasto Mayani.
Mayani alisema kila akiamka asubuhi anakwenda kwa ndugu na jamaa zake, akipata mwenye Sh500 anamsaidia anapeleka ‘nyumbani’ kwa ajili ya kununua chochote cha kupoza njaa .
“Unaweza kwenda kwa mtu akakupa Sh1,000 unanunua unga na kukoroga uji…wakati mwingine kama mzazi nashinda njaa naacha watoto wanakula,” alisema.
Walisema wazazi wengine wanalazimika kupeleka watoto kwa ndugu zao, lakini nao hali zao ni ngumu hivyo wanawarudisha na kuendelea kuishi nao kwenye vifusi vya nyumba zao.
Hali ni ngumu, maisha yamebadilika. Kama nikudhalilishwa tumedhalilishwa kweli mwaka huu, mimi nilikuwa na maisha yangu mazuri, nyumba yangu ilikuwa na duka… nilikuwa nauza napata pesa ya kuweka mfukoni, leo sina kitu nimegeuka ombaomba kwa watu,” alilalamika Simon Magarata.
Magarata anasema: “Leo ninashindia uji huwezi amini, nikiamka asubuhi kitu cha kujiuliza watoto watakula nini, sina kazi ambayo nasema itanisaidia. Kazi yangu ni ya ujenzi wa nyumba, tangu janga limetupata sijasikia hata mtu ananiambia nikamjengee.”
Waathirika hao walidai kuwa tangu walipobomolewa nyumba zao hakuna shirika wala mtu aliyeguswa na hali yao, walau hata kwa kuwasaidia chakula, hata bajeti ya fedha waliyokuwa imeisha. Mwandishi akiwa eneo hilo alishuhudia baadhi ya waathirika hao wakikoroga uji wa sembe na kunywa huku wengine wakichuma mboga za majani, kupika na chakula.
Moris Christopher, baba mwenye watoto wanne aliyekuwa amekaa nao pamoja na mke wake kwenye kibanda walichokijenga juu ya kifusi, aliinamisha kichwa wakati wakila wali uliokuwa umefungwa kwenye mfuko.
“Nina maisha magumu, nawaza sipati jibu. Wamekula jioni najiuliza kesho watakula nini,” alisema.
Alisema tangu alipobomolewa nyumba yake, maisha yake yamebadilika kwani kila siku alikuwa akiamka asubuhi na kuingia mtaani kufanya shughuli zake za kutengeneza sponji na jioni anarudi na fedha kwa ajili ya watoto wake.
“Vifaa vyangu vya kazi vyote vimeharibika baada ya nyumba kubomolewa, sikuokoa hata kijiko kwani wakati wanabomoa sikuwepo, kama unavyoona nikiamka hapa naingia mtaani kuomba, nimeambulia Sh1,500 nimewanunulia watoto wangu wali wanakula,” alisema.

Walalamikia kukosa unyumba
Wazo Mandale akiwa amelala ndani ya kibanda chake alilalamikia ndoa yake kusambaratishwa na watoto wake kuondoka baada ya nyumba yake kubomolewa na kukosa fedha za kuhudumia familia yao.
“Nilikuwa na familia ya watu 15, mke wangu nimempeleka Morogoro na baadhi ya watoto nimewasambaza kwa ndugu, nimebaki mwenyewe, sijui mke wangu atakuwa salama huko aliko,” alisema na kuongeza: “Kitendo cha kukaa mbali na mke ni kibaya kwa walio kwenye ndoa wanajua, ndoa zetu kusema ukweli ziko hatarini kuvunjika,” alisema.
Steven Gwaka, alisema tangu alipobomolewa nyumba yake alihamisha familia na kuipeleka kwa ndugu zake.
“Tupo kwenye upweke wa hali ya juu, mtu umezoea kukaa na familia yako na mke wako, leo hamko pamoja, baba Dar es Salaam mke Morogoro,” alilalamika.

Vyumba bei juu
Hata hivyo wakazi wengine ambao nyumba zimewekewa alama ya X na kuamriwa kuzibomoa wenyewe wamelalamikia vyumba vya kupanga kupanda bei kutoka Sh30,000 hadi Sh70,000 kwa vyumba vya kawaida visivyo na umeme huku vyenye nishati hiyo vikianzia Sh90,000 hadi Sh100,000.
Ismail Said ambaye anafanya kazi ya udalali anasema wenye nyumba wanaangalia fedha kubwa zaidi ya mpangaji.
“Vyumba sasa hivi shida kuvipata, wenye nyumba nao wanaangalia biashara, akiwa na wapangaji wanalipa kodi ndogo anawapandishia kodi kama watashindwa anawaambia watoke,” alisema.
Mwenyekiti wa mtaa wa Kawawa kwenye bonde hilo la Mkwajuni, Elizabeth Masao alisema hali za waathirika hao ni mbaya na kuiomba Serikali na watu wengine wajitokeze kuwasaidia.
“Tuna kaya hapa hazijaondoka, wana hali ngumu, wanaishi kwa kuombaomba, wenye uwezo wanawasaidia walichonacho,” alisema Masao.
Mwananchi








Share on Google Plus

About Mind 2024

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment