MADUDU MAZITO ELIMU YAFICHUKA

NA WAANDISHI WETU

11th January 2016
  Waziri ashtushwa na lugha za walimu, Aahidi mabadiliko ndani ya mwaka.
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako.
Wakati shule zikifunguliwa leo kuanza muhula mpya wa mwaka 2016, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako, amefichua madudu kadhaa katika sekta hiyo.
 
Prof. Ndalichako aliyabaini hayo katika utafiti alioufanya kwa mwaka mmoja na kuapa kuwa atashirikiana na wenzake kufanya marekebisho makubwa katika sekta hiyo.
 
Prof. Ndalichako aliyewahi kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani (Necta) kwa miaka tisa kabla ya kuondoka mwaka 2012, alisema pamoja na mambo aliyobaini, usahihishaji wa kazi za wanafunzi, uadilifu wa walimu na wazazi ni viashiria vibaya kwa elimu nchini.
 
Alisema katika utafiti huo, imebainika kuwa wapo walimu hutumia lugha zisizofaa kwa wanafunzi, mfano ukidhihirishwa na maneno wanayoyaandika baadhi ya walimu kwenye madaftari ya wanafunzi wao baada ya kuwasahihishia mazoezi wanayowapa. 
 
“Naamini maarifa yako kwenye daftari, jinsi mwalimu anavyosahihisha na comments zake zina msaada kwa wanafunzi, kwenye utafiti nilibaini wengi wanatoa comments zinazokatisha wanafunzi tamaa na lugha nyingine za mitaani zisizofaa, kwa mfano, kwenye shule moja nilichukua daftari la mtoto nikakuta mwalimu kamwandikia mwanafunzi ‘vizuri vizuri sana mrembo’… hii siyo sawa,” alisema Ndalichako.
 
Akieleza kuhusu chanzo cha utafiti huo, Waziri Ndalichako alisema kuwa aliamua kuomba likizo bila malipo (wakati akiwa NECTA) na kufanya utafiti huo baada ya kuona wanafunzi wengi wakifanya vibaya katika mitihani yao ya taifa huku  baadhi ya wadau wakitoa majibu ya mkato kuwa mitihani ya baraza hilo ni migumu na kwamba haiendani na kile kilichomo kwenye mitaala ya elimu nchini.
 
“Mwanzoni, wakati watu wanalalamika kuwa mitihani ni migumu, nilikuwa najua siyo dhana sahihi kwa sababu walimu wanaofundisha watoto huko ndiyo waliokuwa wakiitunga (mitihani), na kila swali walilokuwa wakitunga walikuwa wakisema limetoka kwenye syllabus (muhtasari) gani, na mada husika iko ukurasa wa ngapi kwenye syllabus,” alisema Prof. Ndalichako na kuongeza: 
 
“Ikafika mahali tukataka waseme kabisa hiyo mada ipo kwenye kitabu kipi, na ukurasa wa ngapi wa vitabu vile vilivyoidhinishwa kufundishia. Ndiyo maana watu walipokuwa wakilalamika tunatunga mitihani migumu, mara ipo nje ya mitaala, hizo kelele zilikuwa hazinisumbui kwa sababu nilikuwa najua mitihani yetu ni standard (ni ya viwango) na inatoka kwenye mitaala yetu,” alisema. 
 
“Wakati mwingine nilikuwa nawaambia watu kama mitihani ni migumu basi tuanzie kwenye mitaala yetu. Na hilo lilikuwa ni tatizo la muda mrefu, nikaona nipate mwaka mmoja wa kukaa pembeni niangalie sababu hasa zinazofanya wanafunzi wasifanye vizuri,” alisema Prof. Ndalichako.
 
Alisema utafiti wake huo uliojikita kwenye mikoa ya Rukwa, Mbeya, Morogoro, Ruvuma, Mtwara, Lindi na Iringa, ulilenga pia kujua namna walimu walivyokuwa wakipata alama endelevu kwa wanafunzi, ambazo zilikuwa zikitumwa NECTA kwa ajili ya kutumika kwenye mitihani ya mwisho.
 
MADUDU
Akieleza kuhusu utafiti wake huo, alisema alibaini takribani sababu nane kubwa zinazosababisha wanafunzi wasifanye vizuri kwenye mitihani yao ya mwisho.
 
Alisema suala la uadilifu na kufuatwa kwa miiko ya taaluma ya ualimu ni moja ya sababu aliyobaini inachangia kufanya vibaya kwa wanafunzi katika mitihani yao.
 
“Walimu wengine ni wakali mno. Wanafunzi waliniambia kwamba wakati mwingine mwalimu akiuliza swali na mwanafunzi akakosea, mwalimu anamjibu vibaya na siku nzima huyo mwanafunzi hujikuta anakosa amani mbele ya wanafunzi wenzake,” alisema.
 
Akieleza zaidi, alisema jambo hilo hujitokeza hata kwenye madaftari ya wanafunzi ambako ndiko ilikobainika kuwa baadhi ya walimu huwaandikia wanafunzi kwa lugha kali na zisizofaa kutumiwa na walimu.
 
“Ngoja nikupe mifano ya lugha nilizokutana nazo kwenye daftari nilizokagua… ni pamoja na mwalimu mmoja kumwandikia mwanafunzi wake kuwa ‘andika mwandiko mzuri, unakuwa kama mtu ambaye hakunywa chai’,” alisema na kuongeza:
 
“Mwingine anaandika ‘dogo kaza buti’ … hii siyo lugha rasmi, ni ya mtaani… mwingine kaandika ‘dogo ongeza bidii utafeli’. Na yupo mwingine kamwandikia mwanafunzi ‘vizuri sana mrembo’. Sasa (iweje mwalimu) unamwandikia neno mrembo mwanafunzi? Hii inaonyesha jinsi tatizo la jinsi uadilifu linavyotupa changamoto,” alisema Ndalichako.
 
NINI CHA KUFANYA?
Akielezea kuhusu matatizo hayo, Prof. Ndalichako alisema amejipanga kuhakikisha kuwa kwa kushirikiana na wenzake, wanashughulikia matatizo ya aina hiyo kwa ukamilifu ili kuboresha sekta ya elimu nchini.
 
Alisema tayari ameshawaagiza wakaguzi wa shule kukagua madaftari ya wanafunzi wanapoenda shuleni na siyo kukagua majengo kama wanavyofanya sasa.
 
Alisema amebaini kuwa, baadhi ya wakaguzi hawajui ni nini kilicho kwenye madaftari ya wanafunzi kwa kuwa, hujikita zaidi kuangalia miundombinu ya shule badala ya kujua ni nini watoto wanafundishwa.
 
WALIMU KUPOTOSHA WANAFUNZI
Kwa mujibu wa Ndalichako, madudu mengine ni pamoja na baadhi ya walimu kuwapotosha wanafunzi kutokana na kile wanachowafundisha.
 
“Walimu pia wanachangia kupotosha wanafunzi, kuna shule moja nilienda katika kukagua madaftari ya wanafunzi, nikakuta mwalimu kauliza, nini maana ya mazingira? Mtoto mmoja akajibu ‘ni maji na vitendo’, mwalimu akampa tiki (vema), mwingine kaandika ‘ni kuosha vyombo’, pia mwalimu akampa tiki,” alisema.
 
Aliongeza kuwa katika swali hilohilo kuhusu mazingira, kuna mtoto  mwingine kaandika ‘ni usafi’ na mwalimu akampa alama ya vema huku akipata alama ya vema pia kwa jibu kwamba ‘mazingira ni nyimbo’.
 
“Kwa hiyo huyu mwalimu jibu lolote kwake lilikuwa sahihi, na kila mwanafunzi chini kamwandikia ‘vema’… sasa huyu mwanafunzi akija kuandika haya majibu kwenye mtihani wa taifa ni lazima atakosa. Ndiyo maana wazazi wanasema wanafunzi wanafanya vizuri shuleni lakini kwenye mtihani wa taifa wanafanya vibaya, sasa kufanya vizuri kwenyewe ndo huko,” alisema.
 
Hata hivyo, Ndalichako alisema matatizo hayo ya ukosefu wa uadilifu na upotoshaji katika kusahihisha hayako katika kila shule kwani baadhi ya walimu hufanya kazi yao vizuri sana.
 
“Kuna shule moja nilienda nikakuta ina mazingira magumu na hata nyumba ya mwalimu anayoishi haivutii, lakini yeye anasahihisha vizuri na anajitahidi kila mwanafunzi kumpa maoni ambayo yanamsaidia kitaaluma,” alisema.
 
UWEZO WA WALIMU
Prof. Ndalichako alisema uwezo wa walimu pia unatofautiana kwani wapo ambao uwezo wao siyo mzuri, jambo ambalo pia ni changamoto kubwa inayopaswa kufanyiwa kazi.
 
“Wanafunzi wenyewe wanasema baadhi ya walimu hata kujieleza kwa Kiingereza hawawezi, kwa hiyo kuna shule zenye walimu wazuri na nyingine ni kinyume chake na hazifanyi vizuri,” alisema Prof. Ndalichako.
 
WANAOJIUNGA KIDATO CHA KWANZA
Prof. Ndalichako alisema kuwa, kwenye baadhi ya shule alizotembelea, alielezwa kuwa baadhi ya wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza kwenye shule za kata, uwezo wao ni mdogo.
 
“Walimu walisema wanalazimika kutumia muda mwingi kuwapandisha watoto hao kutoka walipo na jambo ambalo hilo huchukua muda mrefu,” alisema.
 
WAZAZI
Mbali na walimu, alisema utafiti wake umebaini kuwa wazazi nao ni sababu ya baadhi ya wanafunzi kufanya vibaya kwenye mtihani wa taifa.
 
“Kuna shule wana walimu wanajituma sana lakini wazazi wanakatisha tamaa na kurudisha mambo nyuma. Kuna sehemu nilienda, walimu wakasema kwamba wakiwaambia watoto waje Jumamosi ili wapate masomo ya ziada ambayo walimu wanatoa bure, wazazi wanakataa na kusema walimu wameshindwa kazi yao kwa sababu wangetakiwa kufundisha kwa ule muda uliotolewa na serikali tu.
 
Kwa hiyo unakuta kuna migogoro mikubwa lakini chanzo chake ni nia njema tu ya walimu kwa wale wanafunzi ambao wamebaini wanahitaji uangalizi maalumu,” alisema, akiongeza kuwa jambo hilo pia watalishughulikia.
 
Aidha, alisema kuna maeneo wazazi huwalazimisha watoto wao wasifaulu mitihani kwa sababu ya kuogopa ghrama za kuwasomesha.
“Sasa elimu bure imeanza, labda itaondoa hicho kisingizio… kwenye utafiti wangu niliambiwa kuwa kwenye baadhi ya shule wazazi wanaenda kuuliza maendeleo ya watoto wao lakini lengo lao siyo zuri, walimu wamegundua hilo na wale wazazi wakienda shuleni inabidi kwanza wachunguze na kujua lengo lao ndipo wawajibu kwa sababu wakiwaambia tu kuwa mtoto anafanya vizuri, wakirudi nyumbani inakuwa vita,” alisema Prof. Ndalichako.
 
NIDHAMU
Alisema nidhamu ni jambo jingine alilobaini kwamba lina mchango mkubwa kwa wanafunzi kufanya vizuri au vibaya.
 
 “Kuna shule moja wanafanya vizuri kweli, kwenye hiyo shule katika uwanja wao wa assemble (wanapokusanyika wanafunzi), kwanza umesakafiwa na umechorwa mistari. Na kwenye hiyo misitari, kila mwanafunzi ana sehemu yake ya kusimama kwa hiyo ni rahisi kujua kuwa hapa alitakiwa asimame nani na leo hayupo, wanafunzi pia wana muda wa kondoka bwenini na hakuna anayeruhusiwa kubaki wenzake wakiondoka.
 
“Nidhamu pia ipo kwa, muda wa kipindi ukifika na dakika tano zikipita kama mwalimu hajaingia wanafunzi wanaenda ofisi ya walimu kumtafuta,” alisema Prof. Ndalichako.
 
Alisema kuwa, kuna shule ambazo walimu wamejifanya miungu watu na wanafunzi hawathubutu hata kumfuata mwalimu hata kama wanahitaji msaada wa kimasomo.
 
“Zile shule ambazo  wanafanya vizuri, walimu wanasimamia taratibu badala ya vitisho kwa hiyo wanafunzi wako karibu na walimu, wanaweza kuwafuata na kuomba msaada wakati wowote,” alisema.
 
MGAWANYO WA WALIMU
Prof. Ndalichako alisema kuwa kwenye shule za serikali, aligundua kuwa kuna mgawanyo wa walimu usio sawa.
 
“Pamoja na kwamba walimu wapo wengi kwa kipindi nilichofanya utafiti niliona kwamba kuna shule kwa mfano zina walimu watatu wa Jiografia lakini hawana mwalimu hata mmoja wa hisabati.
 
Masomo ya Hisabati, Fizikia, Kemia na Bailojia ni changamoto, hilo linachangia pia kwenye matokeo ya wanafunzi,” alisema.
 
Alisema licha ya kuwa suala la uhaba wa walimu lipo Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), watashirikiana kulikabili kwa kuwa mteja wao ni mmoja. 
 
“Uhaba wa walimu wa sayansi utapungua baada ya takribani walimu 5,000 wanaosoma Chuo Kikuu cha Dodoma kuhitimu hivi karibuni. Suala la mgawanyo mbaya ni jambo tu la kuwasiliana na halmashauri husika, tutashughulikia,” alisema.
 
Kuhusu ubora wa walimu, alisema ni wakati wa wakaguzi kuangalia suala hilo kwa umakini.
 
“Tusichukulie tu kwamba mwalimu yupo shuleni, wanapokuwa wanakagua wawe na mbinu za kujua ubora wa walimu wetu,” alisema na kuongeza.
 
“Watu wa kufanya kazi hii wapo, tuna waratibu wa elimu kata, maafisa elimu wilaya, maafisa elimu taaluma, maofisa elimu mikoa na wakaguzi kila wilaya, wapo wa kanda, wote hawa wanalipwa ili wamwangalie mwanafunzi anavyofundishwa.
 
“Mimi sioni sababu kwa nini mwanafunzi anafika darasa la tatu hajui kusoma na kuandika, mratibu elimu kata yuko wapi? Tena wengine wana shule nne tu, na wengine wamepewa pikipiki ili wazunguke shuleni, kwa nini sasa asijue? 
 
Hizi taarifa hazitufikii kwa nini? Wakati mwingine unakuja kujua wakati mwanafunzi yupo darasa la saba. Huu mzigo sitaki kuutupia kwa walimu, labda mwanafunzi ni mzito kujifunza kwa sababu anataka msaada maalumu, lakini pia hata taarifa za hawa wanafunzi hatupati, kwa nini?” alisema.
 
MABADILIKO NDANI YA MWAKA
Pamoja na changamoto alizobaini, alisema anashukuru kupewa nafasi aliyonayo na Rais John Magufuli na kwamba, ndani ya mwaka mmoja, mabadiliko kwenye sekta ya elimu yataanza kuonekana na elimu bora kweli itaonekana.
 
 “Watanzania wategemee kwamba watoto watasoma, nashukuru kwamba Tamisemi wametoa muda ili miundombinu ya kujifunzia kama madawati iwe imewekwa shuleni, dhamira ya dhati ya kuboresha elimu ipo,” alisema.
 
“Lakini tukumbuke kwamba elimu ni uwekezaji, mabadiliko makubwa yawezekana kwenye mwaka huu wa kwanza yasionekana sana lakini  wataona tofauti, wategemee sekta ya elimu kwa ngazi zote itabadilika,” alisema Prof. Ndalichako.
CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About Mind 2024

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment