Dar es Salaam. Licha ya mamia ya watu kujitokeza usiku wa manane kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam kumpokea mshambuliaji Mbwana Samatta, mapokezi hayo yaliingia dosari.
Ni baada ya kutokea vurugu zilizosababishwa na kundi kubwa la vijana waliokuwa wakilazimisha kupiga picha naye.
Hali hiyo ilimlazimu mshambuliaji huyo kutopiga picha, sanjari na kutozungumza na vyombo vya habari na badala yake alifanya hivyo kwenye Hoteli ya Serena alikopumzika baada ya kufika usiku.
Dalili za kutokea kwa hali hiyo zilianza mapema saa 5:00 usiku baada ya vikundi mbalimbali vya watu, hasa vijana kuingia kwenye eneo la uwanja huo wakiwa na ala mbalimbali za muziki zikiwamo ngoma na manyanga, huku baadhi wakiwa wamelewa.
Awali, Serikali, Shirikisho la soka Tanzania (TFF), meneja wa Samatta, Jamal Kisongo pamoja na familia yake waliweka utaratibu maalum ambao ungemwezesha mshambuliaji huyo kuzungumza na waandishi wa habari pamoja na kupiga picha uwanjani hapo.
Utaratibu huo ulishindikana kutokana na vurugu ambazo zilihatarisha usalama wa mshambuliaji huyo pamoja na watu wengine waliojitokeza kumlaki.
Kuwasili
Pamoja na kutolewa taarifa kuwa Samatta angewasili uwanjani hapo saa 8:00 usiku, mshambuliaji huyo alitua nusu baadaye akiwa kwenye ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia. Taarifa za kutua kwa ndege iliyombeba Samatta ziliamsha nderemo na vifijo kwa mashabiki uwanjani hapo walianza kuungana na vikundi vya ngoma vilivyojitokeza kuonyesha furaha yao.
Kabla ya kutoka nje, Samatta alibaki ndani kwa muda kwenye eneo la kupumzikia wageni wanaowasili akiwa na viongozi wa TFF waliojitokeza kwa wingi uwanjani hapo pamoja na Meneja wake Kisongo.
Saa 8.54 usiku, Samatta alitoka nje ya lango la kutokea, ndipo alivamiwa na kundi kubwa la vijana waliogoma kufuata utaratibu uliowekwa, hali iliyowapa wakati mgumu maofisa wa TFF waliokuwa uwanjani hapo kuwadhibiti na hivyo kuvuruga utaratibu.
Tatizo la ulinzi
Hakukuwa na ulinzi wowote wenye kueleweka uwanjani hapo kwani kulikuwa na askari polisi wawili waliovalia sare za jeshi hilo walioonekana kabla ya mshambuliaji huyo kuwasili, ingawa waliyeyuka wakati wa fujo hizo na haikujulikana wapi walipoelekea.
Pia, walinzi wa usalama uwanjani hapo hawakuonyesha juhudi zozote za kuimarisha ulinzi na usalama kabla na baada ya mshambuliaji huyo kuwasili na kuzua maswali kwa watu mbalimbali waliojitokeza kwenye mapokezi hayo.
Yassoda aficha aibu ya Serikali
Licha ya wengi kutarajia kuwa kungekuwepo na baadhi ya viongozi kutoka serikalini, hasa wale wa Wizara ya Michezo, ni Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Maendeleo ya Michezo, Juliana Yasoda pekee aliyekuwapo.
Badala yake kulikuwa na kundi kubwa la maofisa wa TFF wakiongozwa na mkurugenzi wa ufundi, Salum Madadi, mratibu wa timu za Taifa, Martin Chacha, ofisa habari, Baraka Kizuguto, ofisa masoko, Peter Simon, mwenyekiti wa kamati ya sheria na hadhi za wachezaji, Eliud Mvela na ofisa wa mashindano, Idd Mshangama.
Ulimwengu azua taharuki
Mshambuliaji mwenza wa Samatta kwenye timu ya taifa na TP Mazembe, Thomas Ulimwengu nusura asababishe watu wachapane makonde kutokana na kugombea kupiga picha naye wakati alipokuwa anamsubiri Samatta kutua uwanjani hapo. Ugomvi huo ulimalizwa na Ulimwengu aliyewataka mashabiki hao kupiga picha kwa zamu jambo lililofanya ashangiliwe kwa nguvu na kundi hilo la mashabiki.
Zitto aibuka
Mbunge wa Kigoma Mjini wa chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe aliibuka uwanjani hapo saa 8:00 usiku na alizongwa na kundi kubwa la vijana waliokuwa wakimshangilia kabla ya baadaye kwenda kusalimiana na viongozi wa TFF na familia ya Samatta.
Zitto alizungumza na waandishi wa habari kwa ufupi na kusisitiza haja ya kutengenezwa sera ya Taifa ya michezo ili kuibua kina Samatta wengine. Alibeza mfumo wa sasa, akidai kuwa hautoi fursa kwa vipaji vingi kuibuliwa.
“Tunapojivunia mafanikio haya ya Samatta ni lazima Serikali itambue kuwa kunahitajika sera ya michezo kwa Taifa ambayo itakuwa ndiyo mwongozo katika kuwapata Samatta wapya,” alisema Zitto.
Familia ya Samatta
Kwa niaba ya familia, baba mzazi wa mshambuliaji huyo, Ally Samatta alisema kuwa licha ya mwanaye kufanya jambo kubwa na lenye heshima ya kipekee, familia haikupendezwa na utaratibu uliowekwa uwanjani hapo.
“Kama unavyoona tumekuja familia nzima kumlaki, lakini tumeshindwa kufanya hivyo kutokana na hizo vurugu zilizotokea na tunalazimika kwenda hotelini alikofikia jambo, ambalo halipendezi. Hapa uwanjani ndiyo ilikuwa sehemu sahihi kwetu na Watanzania kwa ujumla kupata nafasi ya kumlaki na kupiga picha naye ila ndio hivyo imeshindikana, kwa kweli hatujapendezwa na hili,” alisema.
TFF yawashtukia wapiga dili
Nusura wajanja wanufaike na ujio wa Samatta baada ya kikundi cha watu kuweka bango lenye pongezi kwa mchezaji huyo pamoja na zulia, eneo walilolenga kumsimamisha mshambuliaji huyo kwa ajili ya picha ambazo kila aliyetaka kupiga walitaka kumtoza fedha.
Hata hivyo, hilo lilizuiwa na Yasoda, maofisa wa TFF pamoja na meneja wake Kisongo ambao walidai kuwa wahusika wa mpango huo hawakuwa na kibali maalumu cha kufanya hivyo.
Kauli ya TFF
Shirikisho la Soka Tanzania limewashukuru Watanzania ambao kwa namna moja au nyingine walifanikisha ushindi wa mshambuliaji huyo huku likisema kuwa limejifunza mengi kupitia tuzo ya Samatta.
“Kuna mambo ya msingi ambayo tumejifunza kule Nigeria, lakini kubwa zaidi ni kuwa tuzo zinatolewa kwa yule ambaye anastahili pasipo kuangalia wapi anachezea na anapotokea. Kuna mapendekezo ambayo nitayafikisha mbele ya kamati ya utendaji ambayo naamini yataboresha soka letu,” alisema katibu mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa aliyefuatana na Samatta kwenye tuzo hizo.
Samatta ashukuru
Akiwa hotelini Serena, Samatta aliwashukuru Watanzania kwa kumwombea na kumuunga mkono mpaka ikafanikiwa kuchukua tuzo hiyo.
“Tuzo hii imenipa changamoto ya kufanya vizuri zaidi ili nizidi kuitangaza nchi yangu. Nadhani bado nina safari ndefu kisoka na huu ni mwanzo tu,” alisema Samatta.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment