IMEANDIKWA NA PETI SIYAME, SUMBAWANGA
MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Magalula Said Magalula amesema shule za msingi na sekondari za umma mkoani humo zimepokea zaidi ya Sh milioni 336 kwa ajili ya mpango wa elimu bure.
Magalula alisema fedha hizo zilizotolewa na serikali zitatumika kwa ajili ya mpango wa elimu bure katika shule za msingi na sekondari za umma, ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM na ahadi ya Rais John Magufuli ya elimu bure.
Kwa mujibu wa Magalula, kati ya fedha hizo, kiasi cha Sh 143,859,000 zimepelekwa katika shule za msingi 360 wakati kiasi Sh 212,482,000 zimeshapelekwa katika shule 105 za sekondari.
Mkuu huyo wa mkoa alieleza kuwa kiasi hicho cha fedha kilichotolewa na serikali ni kwa ajili ya mwezi Januari mwaka huu, ambapo kila mwezi serikali itakuwa ikitoa fedha kwa ajili ya mpango huo.
“Nawaagiza wakuu wa shule na walimu wakuu mkoani hapa wahakikishe fedha hizo zinatumika kwa mujibu wa maagizo ya serikali, vinginevyo atakayekwenda kinyume, hatua kali za kinidhamu na kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” alisisitiza.
Hata hivyo, alibainisha kuwa shule mbili za msingi, bado hazijapelekewa fedha hizo kutokana na kutokuwa na akaunti benki. Aliongeza kuwa jitihada zinafanyika kuhakikisha zinafungua akaunti haraka iwezekanavyo.
Akihojiwa, Mkuu wa Shule ya Sekondari Kalangasa Manispaa ya Sumbawanga, Gabriel Hokororo, alikiri kuwa shule yake tayari imepokea Sh 1,400,000 kwa ajili ya mwezi Januari.
Habari Leo
0 comments:
Post a Comment