WATANZANIA WAOMBWA KUMWOMBEA RAIS MAGUFULI

IMEANDIKWA NA MWANDISHI WETU


WATANZANIA wameombwa kumwombea Rais John Magufuli na Serikali yake ya Awamu ya Tano, ambayo inafanya jitihada kubwa za kuondoa kero mbalimbali za wananchi. Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani , maarufu kama ‘Profesa Maji Marefu’.
Alisema hayo alipokutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Alikuwa akitoa maoni yake juu ya mwenendo wa uchapakazi wa Serikali ya Rais Magufuli. Ngonyani aliwataka wananchi wote, bila kujali itakadi zao za kisiasa na dini kuiombea Serikali ya awamu ya tano, ambayo viongozi wake wameonesha uchapakazi wa hali ya juu na kupata mafanikio makubwa katika kipindi kifupi.
Alisema serikali inajitahidi kudhibiti upotevu wa mapato yake na kuziba mianya ya upotevu wa mapato hayo. Aliwahimiza wananchi, waendelee kuunga mkono juhudi hizo ili nchi iweze kupata mafanikio.
“Dini zote zinatakiwa kuendelea kumwombea Rais Magufuli na viongozi wengine wa awamu ya tano ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi na ili kuhakikisha juhudi za Serikali hii ya awamu ya tano hazikwamishwi na watu wachache wanaochukia jitihada zinazofanywa hivi sasa na Serikali,” alisema Ngonyani.
Mbunge huyo wa Korogwe vijijini pia alitoa tahadhari kwa Watanzania kutoacha kumwombea Rais Magufuli, kwani kufanya hivyo kutakwamisha juhudi zake za kutaka kuleta maendeleo ya kweli kwa taifa.
Alisema pamoja na kazi yake kupendwa na kuthaminiwa, kuna baadhi ya watu wachache ambao si waadilifu, ambao walijilimbikizia mali kwa njia zisizo halali, wanamchukia.
“Wanaomchukia Magufuli ni mafisadi, wezi wa mali ya umma, wala rushwa , wafanyabiashara ya dawa za kulevya na wale ambao wamejilimbikiza mali isiyo halali. “Hao ndio maadui wakubwa wa jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano , hivyo Rais na viongozi aliowateua wanahitaji ulinzi wa maombi kwa dini zote na pia kutoka kwa wananchi,” alisema.
Akizungumzia kazi inayofanyika sasa ya kusafisha uozo katika taasisi mbalimbali hapa nchini, Ngonyani alipongeza kazi hiyo na kuitaka Serikali kutoishia hapo ilipofikia sasa. Alitaka nguvu hiyo ielekezwe katika halmashauri za wilaya, ambako nako kuna uozo mkubwa .
“Kwenye halmashauri nyingi hapa nchini, kuna matatizo makubwa na watu wanafanya kazi kwa mazoea , watendaji wa halmashauri na taasisi za Serikali wamejifanya kuwa miungu watu na hivyo kutatiza shughuli mbalimbali za Serikali na huduma kwa wananchi,” alisema.
Aidha, Ngonyani aliiomba Serikali ya Awamu ya Tano kuuangalia mkoa wa Tanga, hasa Jimbo la Korogwe Vijijini ambalo wanan chi wake wana shida mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa ardhi, maji na umeme.
Mbunge huyo alibainisha kuwa katika jimbo lake, ardhi imekuwa ni tatizo kubwa kwa wananchi, kwani mashamba mengi makubwa yamechukuliwa na wawekezaji na kutelekezwa bila kufanyiwa kazi. Hivyo, aliomba kazi ya kutumbua majipu, isiishe Dar es Salaam, bali ifike mikoa mingine hadi vijijini.
Wakati huo huo, Mbunge huyo wa Korogwe vijijini amewataka Watanzania kuacha kumsakama na kumlaumu Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, akisema kufanya hivyo ni kumkosea, kwani alifanya mambo mengi mazuri na Rais Magufuli ni tunda lake, kwani alikuwa ni mmoja wa mawaziri katika serikali yake.
Habari Leo
Share on Google Plus

About Mind 2024

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment