Dodoma/Iringa. Watu wanane akiwamo msaidizi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Mkaguzi wa Polisi, Gerald Ryoba na familia yake wamekufa baada ya kusombwa na maji katika eneo la Kibaigwa wilayani Kongwa baada ya mvua kubwa iliyonyesha katika eneo hilo.
Katika tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia jana katika sehemu maarufu ya Bwawani, mbali na familia ya mkaguzi huyo, miili mingine ya watu wawili ilipatikana katika eneo hilo.
Taarifa inaonyesha kuwa Ryoba na familia yake walikuwa wakitoka mkoani Geita kwenda Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema polisi walipokea taarifa kuwa katika eneo hilo kuna maji mengi yanatiririka kutoka maeneo ya Njoge na Hembahemba na yamesababisha magari kushindwa kupita na pia kuna gari limesombwa na maji hayo.
Taarifa kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa, licha ya magari mengine kushindwa kupita kwa kuhofia wingi wa maji, gari ya polisi huyo lilipofika dereva aliamua kupita, ndipo likasombwa pamoja na abiria wake.
“Baada ya muda tukapokea taarifa kuwa kuna gari limesombwa na maji lakini inaonekana matairi yapo juu, tulianza kufuatilia na tukazuia magari mengine kupita na maji yalipopungua ndipo tukaruhusu magari kupita,” alisema Misime.
Misime alisema walianza hekaheka za kutafuta gari hilo aina ya Toyota RAV 4 na baadaye usiku wa manane walifanikiwa kulipata na walipolitoa kwenye maji walikuta miili ya watu wawili.
Alisema gari hilo lililokuwa lilipondeka walitoa mwili wa Fidea John Kiondo ambaye ni mwalimu wa Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam.
“Baada ya kufuatilia, tukabaini kuwa huyu ni mke wa mkaguzi wa polisi Gerald Ryoba ambaye ni msaidizi wa Afande IGP,” alisema Misime.
Alisema kutokana na taarifa kuwa katika gari hilo kulikuwa na watu sita, waliendelea kutafuta miili mingine na baadaye walipata mwili wa dereva wa gari hilo, F.3243 Koplo Ramadhan ambaye pia alifariki dunia. Miili ya watoto Gabriel Ryoba na Godwin Ryoba na mwili wa mkaguzi Ryoba ilipatikana jana saa 4.20 asubuhi.
Koplo Ramadhani alikuwa mwenyeji wa Mkoa wa Lindi na Ryoba wa Geita, hivyo polisi wanafanya taratibu za kusafirisha miili hiyo kwenye maeneo husika. Mwingine aliyefariki dunia ni msichana wa kazi aliyefahamika kwa jina la Sara, mwenyeji wa Ruvuma.
“Kwa hiyo watu wote sita ambao walikuwa kwenye gari tulifanikiwa kuwapata lakini wakati tunaendelea kutafuta kwenye mkondo huo wa maji tumepata miili mingine miwili, hivyo kuwa na miili ya watu wanane,” alisema Kamanda Misime.
Mwili mmoja umetambulika kuwa ni wa Ofisa Mifugo, Kata ya Pandambili, Kongwa aliyetambuliwa kwa jina moja la Ludege na mwingine haujafahamika.
“Tumeacha maelekezo kwa wananchi ili waweze kutupa taarifa, inaonekana hayo maji yameanzia mbali na yalikuwa mengi. Inawezekana kuna watu wengine pia wamesombwa,” alisema.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Mkoa wa Dodoma, Ibenzi Ernest alisema wamepokea miili sita ya marehemu hao.
Ajali yaua wanne, 35 wajetuhiwa
Katika tukio jingine, watu wanne wamefariki dunia na wengine 35 kujeruhiwa baada ya basi la Luwinzo kugonga lori kwa nyuma.
Kamanda ya Polisi Mkoa wa Iringa, Peter Kakamba alisema ajali hiyo ilitokea jana asubuhi katika Kijiji cha Kinegembasi, Kata ya Mbalamaziwa wilayani Mufindi.
watu wawili walifariki dunia papohapo katika ajali hiyo na wengine wawili walifariki baadaye katika Hospitali ya Makambako wakati wakipatiwa matibabu. Basi hilo lilikuwa likitoka Njombe kwenda Dar es Salaam.
Waliofariki ni Rashidi Kibalabala (47) ambaye alikuwa kondakta wa basi na Salim Changwila (28) na wengine wawili bado hawajatambuliwa.
Majeruhi 33 walipelekwa katika Hospitali ya Mafinga na wengine wawili walipelekwa Makambako kupatiwa matibabu.
Kamanda Kakamba alisema basi hilo lilikuwa kwenye mwendo kasi na lilitaka kulipita lori hilo ambalo lilikuwa limebeba makaa ya mawe, ndipo dereva aliposhindwa na kulivaa kwa nyuma.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mufindi, Innocent Muhagama alisema majeruhi wamepokewa pamoja na miili ya marehemu.
Imeandikwa na Habel Chidawali, Rachel Chibwete na Zainab Maeda
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment