MAGUFULI AMPA CAG 'HESABU'

Rais John Magufuli akizungumza na Mdhibiti na

Rais John Magufuli akizungumza na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Juma Assad (Kushoto) Ikulu jijini Dar es Salaam jana. Picha na Ikulu. 
By Suzan Mwillo, Mwananchi
Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameitaka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ihakikishe Tanzania inaongeza ukusanyaji wa mapato kutoka asilimia 14 ya Pato la Taifa (GDP) hadi kufikia kiwango cha juu zaidi huku akitaka wananchi wafuate sheria.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo jana alipokutana na CAG, Profesa Mussa Assad na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga.
Pia Rais jana alikutana na Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu Abubakar Zubeir na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo.
Akizungumzia mazungumzo hayo, Profesa Assad alisema wamejadili kupunguza gharama za matumizi ya kuendesha Serikali na kuongeza ukusanyaji wa mapato.
Profesa Assad alibainisha kuwa Rais Magufuli ameitaka ofisi yake ihakikishe Tanzania inaongeza ukusanyaji wa mapato kutoka asilimia 14 ya Pato la Taifa (GDP) kwa mujibu wa hesabu za mwaka juzi.
“Hadi mwaka juzi, Tanzania ilikuwa inakusanya mapato kwa kiwango cha asilimia 14 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na Kenya ambayo ilikuwa ikikusanya asilimia 19 ya Pato Taifa na hakuna sababu za msingi kwa nini Tanzania iwe nyuma katika ukusanyaji wa mapato hayo,” alisema Profesa Assad.
Akitoa mrejesho wa mazungumzo hayo, Mganga alisema mazungumzo yake na Rais yalijikita katika mikakati ya namna ofisi ya DPP inavyopaswa kufanya kazi ili kuendana na kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu.”
Mganga alisema wamezungumzia umuhimu wa kuwahimiza Watanzania kufuata sheria na kwamba ofisi yake itatekeleza wajibu wake bila kumuonea mtu.
Kwa upande wake, Muti Zubeir alisema Waislamu nchini wanamuunga mkono na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu Rais Magufuli ili aendelee na juhudi katika utendaji wake wa kazi.
Bulembo alisema Jumuiya ya Wazazi inaunga mkono kazi kubwa inayofanywa na Rais Magufuli na kwamba amemhakikishia kuwa ataendelea kufanya kazi hizo katika kutekeleza Ilani ya CCM.
“Tunafurahi kwamba yapo mambo mengi ambayo Rais Magufuli ameanza kuyatekeleza kwa haraka, mojawapo likiwa ni kufutwa kwa ada za shule na hivi sasa wanafunzi watakwenda shule pasipo kutozwa ada,” alisema.
Mwananchi
Share on Google Plus

About Mind 2024

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment