Usafiri wa mikoani hali bado tete

FRIDAY DECEMBER 24 2021
source: mWANANCHI
New Content Item (1)
By Mwandishi Wetu

Dar/Moshi. Wakati mamia ya wananchi wakiendelea kuhangaikia usafiri katika Kituo cha mabasi cha Magufuli eneo la Mbezi Luis, jijini Dar es Salaam, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) imetoa sababu za kutotoa vibali kwa mabasi madogo (coaster) mwaka huu.

Latra imesema haijatoa vibali hivyo kwa sababu ya fujo zinazofanywa na wamiliki hao, ikiwamo upangaji holela wa nauli.

Imezoelekea kila mwisho wa mwaka, Latra hutoa vibali kwa magari hayo ili kupunguza adha ya usafiri kutokana na ongezeko la abiria linalokuwepo.

Akizungumza na Mwananchi jana, Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Gilliard Ngewe alisema msimu huu hawatatoa vibali kwa magari madogo, kwani yamekuwa chanzo cha fujo na yamekuwa yakijipangia nauli yanavyotaka baada ya kupewa vibali.

Alisema jukumu la Jeshi la Polisi ni kuhakikisha abiria anatoa nauli bila kulanguliwa kwa sababu ni chombo kinachosimamia sheria.

“Kama nauli ni Sh20,000 mtu akatozwa Sh40,000 polisi atakaa pembeni? Kwa hiyo polisi ana inforce sheria zote lakini anayetoa miongozo ya nauli ni kiasi kadhaa ni yule aliyetoa leseni,” alisema Ngewe.




Kuhusu suala la kupanda kwa nauli alisema halijaanza leo, ndiyo maana walitafuta suluhisho la kuzuia watu wasipandishe nauli kiholela kwa kupambana na wapiga debe kwa sababu anayepandisha nauli siyo mmiliki bali mawakala.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mwita Waitara aliliambia Mwananchi kuwa Serikali haijatoa leseni ya msimu na kama kutakuwa na ongezeko la nauli kuna utaratibu wa kutangaza.

“Sasa Polisi na Latra wanatakiwa kusimamia hili badala ya kusimama mlangoni kukagua, kama wanashindwa waajiri vijana kwa muda waulize abiria kama wanatoa kiwango kinachotakiwa,” alisema.

Taboa, Chakua wafunguka

Hata hivyo, mjumbe wa kamati ya utendaji ya Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustafa Mwalongo alisema usafirishaji wa abiria kwa kutumia magari madogo aina ya coaster umekuwa ukiathiri biashara yao.

Alisema magari hayo yanafanya kazi usiku (hakuna kulala) yanapakia abiria maeneo tofauti, yakiwemo Shekilango, Ubungo, Mwenge na Kimara.

Akizungumzia hali ya usafiri, Mwalongo alisema Serikali inatakiwa itafute dawa ya ongezeko la abiria kila ifikapo mwisho wa mwaka, ikiwemo kuacha magari yatembee saa 24 kwa mikoa yenye abiria wengi.

Mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Abiria (Chakua), Hassan Mchanjama alisema Latra kuzuia vibali kwa mabasi madogo aina ya coaster kutasaidia kuzuia upandishwaji wa nauli kiholela.

Alibainisha kuwa magari hayo yatakaporuhusiwa, huleta vurugu, ikiwamo kila mtu kujipangia nauli yake, hivyo kusababisha na mabasi makubwa kupandisha.

Hali ilivyo Kilimanjaro

Wakati Dar es Salaam kukiwa na adha ya usafiri, katika mji wa Moshi ni tofauti, kwani mabasi yanayotoka huko kwenda Dar es Salaam yanakosa abiria, jambo lililochangia kushuka kwa nauli kutoka Sh35,000 hadi Sh15,000.

Mawakala wanabainisha kuwa kukosekana abiria kumefanya mabasi mengi kulazimika kuanza safari na watu kati ya 18 hadi 20 badala 57 kama ilivyokuwa siku za nyuma.

Valeria Tesha, ambaye ni wakala alisema kipindi hiki mara nyingi wamekuwa wakifanya biashara za usafirishaji kwa hasara kutokana na kukosekana kwa wateja.

“Sasa hivi tunafanya biashara kwa hasara kutokana na kukosa abiria, sasa hivi wengi wanashuka hapa wakitokea mikoa mbalimbali, lakini wakati wa kurudi abiria hakuna, wakati mwingine magari yanarudi yalikotoka matupu,” alisema Tesha.

Amani Joseph, ambaye ni wakala wa coaster mjini Moshi alisema licha ya changamoto ya uhaba wa abiria wanayokumbana nayo, kumekuwa na usumbufu barabarani, hasa wasimamizi kutoka Latra ambao wamekuwa wakiwatoza faini kubwa madereva pale wanaposimama barabarani kutafuta abiria.

“Tumekuwa tukipigwa faini kubwa kuanzia Sh250,000 hadi Sh1,000,000 ukikutwa umepaki gari pembeni ukitafuta abiria, hii sio sawa, sisi tunalipa mapato Serikali,” alisema.

Akijibu malalamiko ya madereva hao, Mkurugenzi wa Latra, Johansen Kahatano alisema wingi wa fedha hizo zinatokana na idadi ya makosa ambayo dereva amekutwa nayo.

“Kila kosa lina faini yake, inategemea amekutwa na makosa mangapi, pia wakati anaandikiwa faini anaambiwa makosa yake,” alisema Kahatano.

Wakata tiketi getini wageuza fursa

Wakati hali ya usafiri ukiendelea kuwa shida katika stendi ya Magufuli jijini hapa, abiria wamekuwa wakiibiwa fedha ndogondogo bila ya wao kujua wanapingia ndani ya stendi hiyo.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi ulibaini kuwa baadhi ya abiria wamekuwa wakitozwa hadi Sh400 na wakatisha tiketi za kuingia ndani ya stendi hiyo badala ya Sh200 iliyopangwa.

Hilo hufanywa zaidi na watu hao katika kipindi ambacho kuna idadi kubwa ya watu wanaoingia na kutoka katika stendi hiyo bila wahusika kushtuka.

Mwandishi wa Mwananchi alikutana na hali hiyo kwani baada ya kutoa noti ya Sh1000 kwa mkatisha tiketi huyo alirudishiwa Sh600.

Akijua dhahiri kiingilio ni Sh200 alitoka tena ndani ya stendi hiyo na kulipia tena Sh1000 ambapo alirudishiwa chenji kama ya awali.

Lakini hilo halikumfanya kuridhika kwani aliamua kubadilisha mtu anayekatisha tiketi na kutoa noti ileile na kupewa chenji ya Sh800.

Hali hiyo ilimfanya kwenda kumuuliza kaka aliyekuwa akimpatia chenji pungufu jambo lililomfanya kuomba msamaha na kudai kuwa hakuangalia vizuri na kumuongeza Sh200.

Wakati hilo likiendelea mtu mwingine pia aliyekuwa amepewa chenji pungufu alikuja kudai chenji.

“We kaka mbona umenipa Sh600 kwani kiingilio ni shilingi ngapi,” aliuliza dada huyo ambaye jina lake halikufahamika mara moja.

“Aah… samahani nilichanganya,” alijibu huku akimpatia Sh200 ya kuongezea binti huyo na kuondoka.

Mbali na watu kuibiwa Sh200 lakini pia uchunguzi ulibaini kuwa mapato mengi yamekuwa yakipotea katika eneo hilo kwani abiria wanaokuwa wanaofika stendi hapo kwa ajili ya kukata tiketi za safari siku hiyohiyo wamekuwa hawapewi risiti za malipo jambo linalofanya mapato hayo kutohesabiwa.

Imeandikwa na Fortune Francis, Aurea Semtowe, Tuzo Mapunda (Dar) na Janeth Joseph (Moshi)

Share on Google Plus

About Mind 2024

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment