Waziri Mkuu awasimamisha kazi watumishi wengine watatu TRA
Dar es Salaam. Kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano, imeendelea kuwasomba watendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), baada ya jana Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa kuwasimamisha kazi wengine watatu na kufanya jumla ya waliosimamishwa kuwa tisa.
Watumishi hao wanaofuata nyayo za wenzao akiwamo Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade waliosimamishwa juzi, ni Anangisye Mtafya, Nsajigwa Mwandengele na Robert Nyoni ambao juzi ilielezwa kuwa wangehamishiwa mikoani.
Waziri Mkuu Majaliwa alitoa uamuzi huo jana ili kupisha uchunguzi zaidi wa tuhuma zinazowakabili, akiamuru kama ilivyokuwa kwa wenzao, wasisafiri kwenda nje ya nchi hadi uchunguzi utakapokamilika.
Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Waziri Mkuu jana, ilimkariri Majaliwa akisema, “Kazi ya kuwachunguza ilianza jana ileile (juzi) na sasa tumeona hawa watu wanapaswa kuwa nje ya utumishi ili kupisha uchunguzi ufanyike kwa uhuru zaidi.”
Waziri Mkuu alimuagiza Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Dk Philip Mpango atekeleze maagizo hayo kwa kuwaandikia barua watumishi hao.
Juzi, Waziri Mkuu alifanya ziara ya kushtukiza kwenye Bandari ya Dar es Salaam akiwa na nia ya kukagua namna shughuli zinavyoendelea kwenye bandari hiyo hasa kwenye maeneo ya kupokea mizigo kutoka nje ya nchi.
Katika kikao kilichofanyika bandarini hapo na kuhudhuriwa na baadhi ya viongozi wa Serikali, Waziri Mkuu aliamua kuwasimamisha kazi maofisa watano na TRA kutokana na ‘upotevu’ wa makontena 349 yenye thamani ya zaidi ya Sh80 bilioni.
Waziri Mkuu alisema upotevu huo unasababishwa na mchezo unaofanyika baina ya wafanyabiashara na watumishi wa TRA ambao wanaruhusu makontena kupita bila kulipiwa ushuru na hivyo kuikosesha Serikali mapato.
Saa chache baadaye, Rais Magufuli alitangaza kumsimamisha kazi Bade kutokana na ‘madudu’ hayo na kumteua Dk Mpango kukaimu nafasi hiyo hadi pale uteuzi mwingine utakapofanyika.
Akitangaza uamuzi huo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema Rais pia amezuia safari kwa watumishi wote wa TRA ili watoe ushirikiano katika uchunguzi wa sakata hilo.
“Mnakumbuka kuwa Rais alisema atatumbua majipu, hilo ni jipu la kwanza lakini bado uchunguzi unaendelea. Watasimamishwa zaidi kadri uchunguzi unavyoendelea,” alisema.
Waliosimamishwa juzi ni Kamishna wa Kodi na Forodha wa TRA, Tiagi Masamaki na Habibu Mponezya wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja, Haruni Mpande na Hamis Ali Omari wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano pamoja na Eliachi Mrema wa Kitengo cha Bandari Kavu (ICD).
Wakamatwa, pasipoti zazuiliwa
Katika kutekeleza maagizo, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athmani alisema kuwa amri ya Waziri Mkuu Majaliwa ya kuwakamata maofisa watatu wa TRA, imetekelezwa na tayari wahusika wamekamatwa pamoja na kuzuia pasipoti zao.
Alisema agizo hilo limetekelezwa mara moja na upelelezi zaidi wa watuhumiwa unaendelea ili kubaini mambo mengi dhidi yao kabla ya kuendelea na hatua nyingine.
Alipoulizwa kuhusu hati zao za kusafiria, alijibu, “Kuzuia hati zao na kuwakamata ni jambo dogo, ukilinganisha na upelelezi unaoendelea dhidi yao, tumeshawakamata na mambo mengine yanaendelea, kwa sasa sina la kuongeza kwa sababu nitakuwa natoa siri za upelelezi,” alisema DCI Diwani.
0 comments:
Post a Comment