MBUNGE wa Viti Maalumu mkoa wa Mara, Joyce Sokombi kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) amempongeza Rais John Magufuli, kwa kasi yake ya kuwawajibisha watu na watumishi wa serikali wanaojinufaisha na mali ya umma.
Mbunge huyo alisema kasi ya Rais Magufuli inaridhisha kwa kuwawajibisha watu na watumishi wa serikali wanaohujumu mali za umma na kwamba Chadema, siku zote imekuwa ikisisitiza watu kuwajibika kwa kufanya kazi halali na siyo kuhujumu mali za umma kwa manufaa yao binafsi.
Sokombi aliyasema hayo jana mjini Bunda wakati akizungumza na wenyeviti na makatibu wa chama hicho katika majimbo ambayo Chadema iliyapoteza katika Uchaguzi Mkuu uliopita ambayo ni Mwibara, Butiama, Musoma, Bunda na Musoma Vijijini, Kikao ambacho kilikuwa ni kwa ajili ya kufanya tathmini ya uchaguzi huo.
Alisema siku zote kaulimbiu ya Chadema ni watu kufanya kazi halali na siyo kuiba mali za umma kwa maslahi yao binafsi na kwamba sasa uchaguzi umekwisha kinachotakiwa kwa wananchi wa mkoa wa Mara ni kufanya kazi za kujiletea maendeleo na sio kuiba na kujinufaisha na mali ya umma.
“Siku zote sisi Chadema tumekuwa tukipinga ufisadi na wizi wa mali ya umma, kinachotakiwa ni kufanya kazi halali na siyo kuiba na kujinufaisha na mali ya umma… uchaguzi umeisha wananchi sasa tufanye kazi za kujiletea maendeleo,” alisema.
Aidha, mbunge huyo aliwaomba viongozi wa chama hicho katika majimbo yote ya Mkoa wa Mara kujenga tabia ya kufanya vikao vya ndani vya mara kwa mara ili kukijenga na kukiimarisha chama.
Katika hatua nyingine, mbunge huyo aliwaomba wananchi wote mkoani Mara bila kujali itikadi zao za vyama vya siasa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na kusema kuwa yeye ni mbunge wa wananchi wote wa mkoa huo, kauli ambayo pia iliungwa mkono na Katibu wake, Manyumba Idd.
“Mbunge wetu ni mbunge wa wananchi wote na sisi tutamsaidia kwa karibu zaidi ili kuhakikisha anatekeleza wajibu wake wa kutumikia wananchi wote wa mkoa wa Mara, na Tanzania kwa ujumla,” alisema Idd. N
Source: Habari Leo
0 comments:
Post a Comment