UTAFITI: TANZANIA IKO SALAMA

TAASISI ya Utafiti ya Twaweza imezindua matokeo ya utafiti walioufanya hivi karibuni ukionesha asilimia 88 ya Watanzania wanaiona Tanzania iko salama. Matokeo ya utafiti huo wenye jina ‘Itikadi kali inavuma Tanzania’, yametokana na takwimu za sauti za watu 1,879 zilizopatikana kwa njia ya simu za mkononi kati ya Septemba 2 na Oktoba 11, mwaka huu .
Akizungumzia utafiti huo jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze alisema utafiti huo ni wa kwanza Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa. Alisema licha ya hisia kwamba kwa sasa Tanzania iko salama, asilimia tano watu bado wana wasiwasi juu ya vitisho vya mashambulizi katika siku zijazo.
Alisema matokeo ya utafiti yanaonesha wananchi wanaamini kuwa ukosefu wa ajira, utawala mbovu pamoja na kukatishwa tamaa na mifumo ya serikali ndio vitu vinavyochangia kuibuka kwa makundi yenye itikadi kali, Afrika Mashariki .
Asilimia 21 ya wananchi wanadhani kuwa dini inaweza kuwa sababu. “Kwa picha hii na hali halisi ya nchi yetu hatushangai kuona kwamba wananchi wanahofia uwezekano wa mashambulizi kutokea lazima tuangalie jambo hili kwa makini zaidi,” alisema Eyakuze.
Alisema utafiti huo umeonesha asilimia 46 ya wananchi wana wasiwasi juu ya vikundi vyenye itikadi kali kujaribu kuwashawishi wanafamilia kujiunga. Wengine wanahofia wanafamilia wao kushawishika kujiunga navyo na asilimia tano ya wananchi wanamjua mtu ambaye amejiunga au aliyeshawishiwa kujiunga na vikundi hivyo.
Aliongeza kuwa utafiti huo pia umeonesha asilimia 48 ya wananchi wanapendelea ufumbuzi wa kijeshi kupambana na vikundi vyenye itikadi kali na asilimia 20 wanapendekeza mazungumzo na vikundi hivyo kama njia bora katika kusonga mbele.
Hata hivyo, asilimia 96 ya wananchi wana imani kubwa na jeshi wakiliona imara huku asilimia 90 wakiwa na imani kwamba linaweza kuwalinda dhidi ya shambulizi lolote. “Imani hii kwa vyombo vya usalama vya nchi imechangiwa na hisia za wananchi kuhusu serikali kufanikisha kudumisha usalama wakati wa uchaguzi inaonesha asilimia 61 walifikiri serikali ilifanya kazi kubwa kudumisha usalama katika kipindi hicho,” aliongeza Eyakuze.
Alisema kihistoria polisi siku zote wamekuwa wakitazamwa vibaya na wananchi, kwani asilimia 61 ya wananchi waliitaja kama taasisi kinara wa rushwa nchini na dosari zao kadhaa ndio sababu kuu zinazofanya uhalifu kutoripotiwa Polisi.
Akizungumzia matokeo ya utafiti huo, Mkuu wa Usalama Jeshini, Meja Jenerali Venance Mabeyo alisema suala la itikadi kali ni pana, hivyo jamii inatakiwa kuondoa tofauti zao. Alisema tishio la mashambulizi si kubwa kama nchi nyingine na linaweza kumalizika kabla halijaleta madhara.
“Tanzania bado haina makundi ya kigaidi, mengi ni ya kijamii wananchi wasiwe waoga, hali inadhibitiwa na wananchi wanatakiwa kuwa watoa taarifa za matukio hayo ili isaidie jeshi,” alisema Meja Jenerali Mabeyo.
Habari Leo
Share on Google Plus

About Mind 2024

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment