Ni Mabadiliko
* Magufuli ampeleka Maswi TRA
* Majenerali JWTZ wapewa wizara nyeti
RAIS Dk. John Magufuli amemteua Katibu Tawala Mkoa wa Manyara, Eliakimu Maswi, kuwa Kaimu Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kutengua uteuzi wa aliyekuwa anashika wadhifa huo, Lusekelo Mwaseba ambaye atapangiwa kazi nyingine.
Kabla ya uteuzi huo, Maswi alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, lakini alisimamishwa kutokana na tuhuma za uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow, kabla ya kusafishwa na tume iliyoundwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete na kuteuliwa kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Manyara.
Mbali na uteuzi huo, Rais Magufuli amefanya uteuzi wa makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu katika wizara mbalimbali, huku akiwaacha makatibu wakuu kadhaa.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Dar es Salaam jana, ilisema katika uteuzi huo, Rais Magufuli ameteua makatibu wakuu 29 na naibu makatibu wakuu 22.
Katika uteuzi huo, Rais Magufuli amemteua Balozi Ombeni Sefue kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Peter Ilomo, Katibu Mkuu Ikulu na Dk. Laurian Ndumbaro, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora.
Katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhandisi Mussa Iyombe ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Dk. Deo Mtasiwa (Naibu Katibu Mkuu – Afya) na Bernard Makali (Naibu Katibu Mkuu – Elimu).
Ofisi ya Makamu wa Rais, Katibu Mkuu ni Mbaraka Wakili na naibu wake ni Mhandisi Ngosi Mwihava.
Rais Magufuli amewateua makatibu wakuu watatu katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge, Sera, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu) ambao ni Erick Shitindi (Katibu Mkuu Kazi na Ajira), Mussa Uledi (Katibu Mkuu Bunge) na Dk. Hamis Mwinyimvua (Katibu Mkuu – Sera).
Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi pia ameteua makatibu wakuu watatu ambao ni Dk. Frolence Turuka (Katibu Mkuu – Kilimo), Dk. Mashingo (Katibu Mkuu Mifugo) na Dk. Budeba (Katibu Mkuu – Uvuvi).
Kwa upande wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, itaongozwa na Mhandisi Joseph Nyamuhanga (Katibu Mkuu – Ujenzi), Dk. Leonard Chamuliho (Katibu Mkuu – Uchukuzi), Profesa Faustine Kamuzora (Katibu Mkuu – Mawasiliano) na Mary Sassabo (Naibu Katibu Mkuu Mawasiliano).
Taarifa hiyo imesema Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itaongozwa na Katibu Mkuu, Dk. Yamungu Kayandabira na naibu wake, Dk. Moses Kusiluka, wakati Wizara ya Maliasili na Utalii itaongozwa na Katibu Mkuu Meja Jenerali Gaudence Milanzi na Anjelina Madete (Naibu Katibu Mkuu).
Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji itakuwa na makatibu wakuu wawili, ambao ni Dk. Adelhem James Meru (Katibu Mkuu – Viwanda) na Profesa Adolf Mkenda (Katibu Mkuu – Biashara na Uwekezaji) ambaye naibu wake ni Mhandisi Joel Malongo.
Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, itaongozwa na Katibu Mkuu Maimuna Tarishi akisaidiwa na naibu makatibu wakuu wawili, Profesa Simon Msanjila na Dk. Leonard Akwilapo, huku Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, itaongozwa na Katibu Mkuu Afya, Dk. Mpoki Ulisubisya.
Kwa upande wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, makatibu wakuu ni Sihaba Nkinga na Profesa Elisante Ole Gabriel Mollel, huku Nuru Mrisho akiteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu.
Katika Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Mbogo Futakamba amebaki kwenye nafasi ya Katibu Mkuu na naibu wake ni Mhandisi Kalobero Emmanuel.
Wizara ya Nishati na Madini imepata mabadiliko baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu, Omar Chambo kuondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Profesa Justus Ntalikwa, huku akisaidiwa na manaibu Profesa James Mdoe na Dk. Paulina Pallangyo.
Wizara ya Katiba na Sheria, Katibu Mkuu wake ni Profesa Sifuni Mchome, akisaidiwa na manaibu wawili, Suzan Mlawi na Amon Mpanju.
Kwa upande wa Wizara ya Mambo ya Ndani itaongozwa na Katibu Mkuu Jaji Meja Jenerali Projest Rwegasira na naibu wake ni Balozi Hassan Yahaya.
Wizara ya Fedha na Mipango imeachiwa Katibu Mkuu yule yule Dk. Silvacius Likwelile ambaye sasa atakuwa na manaibu watatu ambano ni Dorothy Mwanyika, James Dotto na Amina Shaban, wakati Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Katibu Mkuu ni Dk. Aziz Mlima na naibu wake ni Balozi Ramadhan Mwinyi.
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Katibu Mkuu wake ni Job Masima na naibu wake ni Immaculate Peter Ngwale.
Taarifa hiyo ilisema makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu wote ambao wameachwa katika uteuzi huo watapangiwa kazi nyingine.
MASWI
Kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 250 ilisababisha Maswi aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini asimamishwe mwishoni mwa Desemba mwaka jana.
Mbali na Maswi, aliyekuwa waziri wake, Sospeter Muhongo pia alisimamishwa pamoja na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
Mei mwaka huu, Balozi Sefue alibainisha kuwa uchunguzi uliofanywa kuhusu tuhuma za Maswi kuhusika kwenye sakata la akaunti ya Tegeta Escrow, umebainisha hana hatia na hajahusika kwa namna yoyote kwenye kashfa hiyo.
Alisema uchunguzi huo umeonyesha hakuna ushahidi wa moja kwa moja uliomtia hatiani Maswi, Profesa Muhongo na mawaziri wengine wanne ambao waliong’olewa na Bunge baada ya majina yao kutajwa katika kashfa ya Operesheni Tokomeza.
Aliongeza kuwa Maswi alikuwa akichunguzwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Kamati ya Uchunguzi wa Awali ya Mamlaka ya Nidhamu ambazo zote hazikumkuta na hatia wala ukiukwaji wowote wa maadili ya viongozi wa umma.
Ripoti za uchunguzi huo zilibaini alichokifanya Maswi kilizingatia matakwa ya sheria, ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na ridhaa ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO), hivyo hakuna kosa linaloweza kumfanya afunguliwe mashtaka ya kinidhamu akidaiwa kuruhusu utoaji fedha zilizokuwa katika akaunti hiyo.
Balozi Sefue alisisitiza kuwa Maswi alitenda kazi yake kwa kiwango kinachoridhisha kwa kufanya mawasiliano na mamlaka mbalimbali kwa nyakati tofauti na hakuwa miongoni mwa watu waliopata mgawo wa fedha au fadhila yoyote.
Alisema Profesa Muhongo naye hana hatia kwani wakati Maswi akichunguzwa, naye walikuwa wakimchunguza ndiyo maana kuna baadhi ya watu walipelekwa kwenye Baraza la Maadili kuhojiwa, lakini yeye hakupelekwa.
Ripoti za uchunguzi huo zilibaini alichokifanya Maswi kilizingatia matakwa ya sheria, ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na ridhaa ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO), hivyo hakuna kosa linaloweza kumfanya afunguliwe mashtaka ya kinidhamu akidaiwa kuruhusu utoaji fedha zilizokuwa katika akaunti hiyo.
Balozi Sefue alisisitiza kuwa Maswi alitenda kazi yake kwa kiwango kinachoridhisha kwa kufanya mawasiliano na mamlaka mbalimbali kwa nyakati tofauti na hakuwa miongoni mwa watu waliopata mgawo wa fedha au fadhila yoyote.
Alisema Profesa Muhongo naye hana hatia kwani wakati Maswi akichunguzwa, naye walikuwa wakimchunguza ndiyo maana kuna baadhi ya watu walipelekwa kwenye Baraza la Maadili kuhojiwa, lakini yeye hakupelekwa.
Tanzania Today,
0 comments:
Post a Comment